March 12th, 2012
Nguruwe
ni mnyama mwenye faida, ni rafiki kwa mazingira na hahitaji gharama kubwa
“Ufugaji wa Nguruwe ni lazima uwe wa kisasa ili kupata
mazao bora. Unaweza kupata kila unachohitaji wewe, familia na hata ndugu zako
kutokana na ufugaji wa nguruwe”, anasema Bwana Lomaiyani Molel kutoka
Arusha. Jamii nyingi hapa Tanzania huchukulia nguruwe
kama mnyama mchafu na asiyefaa kuwa karibu naye na hata kwa matumizi kama
lishe. Zaidi, nyama yake inapendwa na haina madhara kwa afya na inapendekezwa
kuliwa zaidi kuliko nyama nyekundu. Unaweza kuanzisha mradi wa nguruwe kwa
gharama ndogo lakini baada ya kipindi cha miezi tisa tu ukaanza kujipatia
kipato kutokana na ufugaji huo.
Ufugaji
Kwa
kawaida nguruwe wanafugwa na watu wa kada zote, wafugaji wadogo wadogo na hata
wakubwa. Aina hii ya ufugaji huweza kumpatia mkulima kipato pamoja na lishe kwa
familia, na hauhitaji gharama kubwa.
Banda
Nguruwe wanahitaji kuwa na banda lililojengwa kwa vifaa
nafuu. Unaweza kutumia mchanga na simenti kuweka sakafu, ama ukatumia udongo wa
mfinyanzi kwa ajili ya kuweka sakafu. Ukubwa wa banda unategemeana na idadi ya
nguruwe unaotaka kufuga. Mita 3 kwa mita 2.5 zitawaweka guruwe 8-10
wanaonenepeshwa kwa soko au nguruwe jike mmoja na nguruwe ndume mmoja.
Malisho
Ulishaji
wa nguruwe ni rahisi kwa kuwa wanakula aina mbalimbali za vyakula kulingana na
mazingira wanayofugwa. Unaweza kuwalisha kwa kutumia majani laini ya aina
mbalimbali, na pia hulishwa kwa kutumia masalia ya nafaka (pumba). Unaweza
kuwalisha kwa kutumia mashudu au pumba aina ya Wheat Poland. Pia unaweza
kuwalisha kwa kutumia mabaki ya jikoni.
Kuzaliana
Nguruwe hubeba mimba kwa kipindi cha siku 114, ambazo
hugawanyika kwa miezi 3, wiki 3 na siku 3. Nguruwe mmoja ana uwezo wa kuzaa
watoto 6 hadi 14 kwa mara moja. Watoto wa nguruwe (piglets) huanza kula chakula
cha kawaida wanapofika umri wa mwezi mmoja na nusu mpaka miezi miwili. Endapo
nguruwe watapata matunzo mazuri, baada ya miezi 8 wanakuwa na uzito kati ya
kilo 50-70 na wanaweza kuuzwa.
Matunzo
Baada
ya nguruwe kuzaa anatakiwa kupatiwa chakula cha kutosha na cha kutia nguvu ili
kupata maziwa ya kutosha kwa ajili ya watoto wake. Watoto wa nguruwe wachomwe
sindano ya madini ya chuma (Iron injection) baada ya siku moja au mbili toka
kuzaliwa. Hii ni muhimu sana vinginevyo wanaweza kufa wote. Kata meno (tooth
clipping) baada ya miezi mitatu. Unaweza kuhasi madume (castration) baada ya
miezi miwili.
Magonjwa yanayoathiri
nguruwe
Kuna
aina nyingi za magonjwa yanayoshambulia nguruwe, lakini yapo yale yaliyozoeleka
ambapo ni lazima kukabiliana nayo ili kuwa na ufugaji wenye tija.
Ugonjwa wa miguu na
midomo
Ugonjwa
huu huathiri nguruwe sehemu za miguu na midomo. Ni ugonjwa ambao hushambulia
nguruwe mara kwa mara hasa wasipokuwa na matunzo mazuri. Ugonjwa wa miguu na
midomo, hudhoofisha nguruwe kwa haraka sana, ikiwa ni pamoja na kupungua uzito.
Chanjo: Chanjo kwa ajili ya
ugonjwa wa midomo na miguu (FMD vaccine) hutolewa kila baada ya mwaka
mmoja. Hii inasaidia kuwaweka nguruwe wako katika hali nzuri zaidi bila
kushambuliwa na magonjwa hayo.
Tiba:
Ugonjwa
huu hauna tiba halisi. Inapotokea nguruwe wakawa wameshambuliwa
kinachofanyika ni kutibu magonjwa nyemelezi kwa kutumia antibiotics.
Homa ya Nguruwe
(Swine fever)
Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya nguruwe huenea
kwa haraka sana miongoni mwa makundi ya nguruwe, na huua kwa haraka sana,
lakini hauna madhara kwa binadamu na hauambukizwi kwa binadamu. Nguruwe
walioambukizwa
waanshikwa
na vindonda ama mapunye kwenye ngozi. Pia masikio na ngozi huwa mekundu.
Chanjo:
Ugonjwa
huu hauna chanjo wala tiba. Kinachofanyika mlipuko unapotokea ili kuwa
salama ni kuwateketeza nguruwe wote walioathirika na kuanza upya. Unaweza
kuteketeza kwa kuwachoma moto.
Muhimu: Baada ya kuwateketeza
nguruwe wagonjwa, safisha banda kisha nyunyiza dawa aiana ya Acon au
Ectomin, na uache banda wazi kwa kipindi cha wiki moja kabla ya kuweka nguruwe
wengine.
Ugonjwa wa mapafu
(Pneumonia)
Huu
ni ugonjwa unaoshambulia sehemu za koo na mapafu ya nguruwe, ambapo husababisha
kukohoa na kupumua kwa shida. Ugonjwa huu husababishwa na bacteria (Secondary
bacterial), joto kupita kiasi, vumbi na gesi inayotokana na madawa makali.
Tiba:
Homa
ya mapafu kwa nguruwe inatibika kwa kutumia antibiotics. Pamoja na kuwaweka
wanyama sehemu safi, isiyo na baridi kali au joto la kupitiliza kiwango.
Kimeta (Anthrax)
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria wanaojulikana
kama Bacillus anthracis, wadudu hawa wanabaki kuwa hai kwa muda mrefu na
wanaweza kuwa kwenye udongo wakiwa hai kwa kipindi cha miaka mingi.
Chanjo:
Chanja
nguruwe wako dhidi ya kimeta kama utakavyoelekezwa na wataalamu wa
mifugo walio karibu nawe.
Tiba: Unaweza kutibu
nguruwe wako kwa kutumia dawa aina ya Penisilin au
Oxytetracycline.
Muhimu:
Homa
ya nguruwe ni lazima iwekewe karatini kwa sababu husambaa kwa haraka
sana. Nchini Tanzania mlipuko wa homa ya nguruwe umekuwa ukitokea mara kwa mara
maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Malawi na katika mkoa wa Mbeya.
Ushauri: Kwa ushauri zaidi juu
ya ufugaji wa Nguruwe na magonjwa ya wanyama,
unaweza
kuwasiliana na Mtaalamu wa mifugo Bwana Oletikoishi Wawaa, simu 0754
207 987.